KANDANDA NI BURUDANI


Shukuruni kwa Muumba, mtoa vyote vipaji

Kila kitu kakiumba, hata hao wachezaji

Basi nami ninaimba, nikipambwa na mataji

Hongereni wachezaji, kwa kuonyesha viwango.

 

Mchezo nauchambua, pasipo hata bakiza

Kipa la shule lajua, magoli kuyakataza

Michomo kaipangua, hata na ya kwenye kiza

Majina nayapaisha,  ndiye Jose mwana Marko .

 

Mabeki wao visiki, utaja ngoka misuli

Usijenge urafiki, hakika hutanawili

Wao hawataki kiki, wakaba hata vivuli

Fard, Ngomela, Lisaku, Alex wote ‘metisha.

 

Ufundi upo dimbani, wanaume kupambana

Chenga zile za utani, mashati kukamatana

Nyasi kwenda mdomoni, Itimba kashindikana

Rweyemamu katikisa, Avit mwamba wa Bongo.

 

Utamu na burudani, winga zote kuteleza

Kwa upepo wa kifani, Myeya awabuluza

Aingia hadi ndani, goli zuri jimaliza

Magoli ni burudani, wa mchezo wa kandanda.

 

Tisa kumi hazikai, zinawinda kama Simba

Golini hazipotei, tele zipo zimevimba

Ntungwa naye hapoi, Bunami naye atamba

Magoli kuyamimina, kutoka kwa Usangira .

 

Burudani ya kutosha, vifijo nje na ndani

Gozi laombwa kuisha, wamechoka wapinzani

Ndo utamu wa maisha, kupokea burudani

Mpira ni uungwana, makocha wapongezana.

Na Stanislaus Stephan Usangira

+2557143258976/+255694091955

stanislausstephan8@gmail.com

Bukoba-Tanzania .

Previous MPs recommend halving of fuel taxes
Next THE KEY TO ALIGNING YOURSELF TO GOD Pt 3

No Comment

Leave a reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *